WAZIRI MKUCHIKA ARIDHISHWA NA MAFANIKIO YA WALENGWA WA TASAF WILAYANI LIWALE.

User Rating: 0 / 5

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,Mheshimiwa George Mkuchika amesema Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaotekelezwa na Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF- ni mojawapo ya vielelezo vya mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya 2015 inayoelekeza serikali na Wananchi kukabiliana na umaskini.

Waziri Mkuchika ameyasema hayo akiwa katika wilaya ya Liwale Mkoani Lindi ambako pamoja na mambo mengine anakutana na Walengwa wa TASAF ili kujionea namna Walengwa hao wanavyotumia fursa zilizoko kwenye Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kujiletea maendeleo na kupunguza athari za umaskini miongoni mwao.

“kote nchini ninakofanya ziara kukagua shughuli za TASAF ninashuhudia mabadiliko makubwa katika maisha ya Walengwa jambo ambalo ni zuri na linapaswa kuendelezwa” amesisitiza Mhe. Mkuchika.

Aidha Waziri huyo ametaka Wataalam wa sekta mbalimbali nchini kote kuwa karibu zaidi na Wananchi na hususani Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ili waweze kuboresha zaidi maisha yao na kunufaika na jitihada za serikali.

Akiwa katika kijiji cha Mbonde Katika wilaya ya Liwale Waziri Mkuchicha alitembelea baadhi ya kaya za Walengwa na kujionea namna wanavyotumia ruzuku itolewayo na TASAF katika kuboresha makazi kwa kununua mabati na kuezeka nyumba zao huku wengine wakianzisha shughuli za uzalishaji mali kama ufugaji wa kuku,bata, na kukuza shughuli za kilimo na hivyo kujiongezea kipato.

Kuhusu sekta ya afya,Waziri Mkuchika amekagua jengo la zahanati lililojengwa na TASAF kwa kushirikiana na Wananchi katika kijiji cha Mbonde zahanati ambayo imewaondolea wakazi takribani 400 adha ya kufuata huduma za matibabu mbali ya kijiji chao.Amewaasa Wananchi hao kulitunza jengo hilo ili waendelee kunufaika nalo.

Mapema Waziri Mkuchika akizungumza na Watumishi wa Umma waliopo katika Wilaya ya Liwale,aliwataka watekeleze majukumu yao kwa kuzingatia msingi ya uadilifu na kujituma ili kuondoa kero za wananchi huku akionya kuwa kamwe serikali haitawavumilia Watumishi wanaokiuka misingi ya utawala bora kwa namna yoyote ile.

 pic1

Waziri Mkuchika (mwenye shati jeupe)akiwa katika nyumba ya mmoja wa Walengwa (kulia kwake)katika kijiji cha Mbonde ,nyumba ambayo imezekwa kwa mabati baada ya kupata ruzuku kutoa TASAF.

pic2

Waziri Mkuchika akipata maelezo ya namna jengo la zahanati lililojengwa na TASAF katika kijiji cha Mbonde, Wilayani Liwale mkoani Lindi linavyowanufaisha wananchi wa eneo hilo na vijiji vya jirani.

pic3

Waziri Mkuchika akizungumza na Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaotekelezwa na Serikali kupitia TASAF katika kijiji cha Mbonde (picha ya chini).

pic4

MAAFISA WA DRC WAWASILI NCHINI KUJIFUNZA SHUGHULI ZA TASAF.

User Rating: 0 / 5

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive

Ujumbe wa Maafisa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo-DRC- umewasili nchini kwa ziara ya siku 10 kujifunza namna Serikali ya Tanzania kupitia Mfuko wa Maendeleo ya jamii –TASAF ilivyofanikiwa kutekeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini-PSSN.

Akiwakaribisha Maafisa hao kwenye Ofisi ndogo za TASAF jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko huo Bwana Ladislaus Mwamanga amebainisha hatua mbalimbali zilizochangia kufanikiwa kwa Mpango huo wa Kunusuru Kaya Maskini unaohudumia Zaidi ya Kaya Milioni MOJA NA LAKI MOJA nchini kote.

Bwana Mwamanga amesema mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa shughuli za Mfuko huo yametokana na ushirikishwaji wa jamii huku akisema mchango wa Serikali ya Tanzania na Wadau mbalimbali za Maendeleo umechangia kwa kiwango kikubwa kufanikisha Mpango huo wa aina yake kupata kutekelezwa nchini.

Mkurugenzi Mtendaji huyo wa TASAF amewaambia Maafisa hao kutoka DRC kuwa Mfuko huo tangu kuanzishwa kwake umejikita zaidi katika kuboresha huduma za kijamii hususani katika sekta za elimu, afya,maji,mazingira,na kuhamasisha walengwa kuanzisha shughuli za uzalishaji mali ili waweze kukuza uchumi na kupunguza umaskini.

Kwa upande wake kiongozi wa ujumbe huo bwana Ruphin Kimuemue Bo- Elongo amesema lengo la ziara hiyo ni kujifunza namna serikali ya Tanzania kupitia TASAF ilivyofanikiwa kuwahudumia wananchi hususani wanaoishi katika hali ya umaskini .

Amesema wamevutiwa na mafanikio ambayo TASAF imeyapata katika utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ambao wamesema utaisaidia pia DRC kutokana na kuwa na wananchi wake wengi wanaishi katika adha ya umaskini.

Ukiwa katika ofisi za TASAF ujumbe huo umepata fursa ya kufahamishwa utekelezwaji wa shughuli za taasisi hiyo zikiwemo za Ajira za Muda ,Uhawilishaji Fedha, na Uwekaji wa Akiba kwa Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.

Maafisa hao kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo pia watatembelea wilaya ya Kibaha mkoani Pwani ,Temeke na Zanzibar ambako watakutana na Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini na kujionea namna wanavyonufaika na huduma za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii –TASAF.

 pic1

Ujumbe kutoka DRC ukimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF,(anayeitazama kamera) kwenye ukumbi wa ofisi ndogo ya TASAF jijini DSM.

pic2

pic3

Mkurgenzi Mtendaji wa TASAF,Bw. Ladislaus Mwamanga (wa tatu kulia ) akiwa katika picha ya pamoja na ujumbe kutoka DRC ambao uko nchini kujifunza shughuli za huduma ya hifadhi ya jamii

 

DR.MARY MWANJELWA AVUTIWA NA MPANGO WA KUNUSURU KAYA MASKINI UNAOTEKELEZWA NA TASAF.

User Rating: 0 / 5

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ,Dr. Mary Mwanjelwa ameuagiza Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF kuendelea na Utaratibu bora zaidi wa kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa shughuli za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ili Wananchi waweze kunufaika na Mpango huo ulioanzishwa na kutekelezwa na Serikali.

Dr. Mwanjelwa ametoa agizo hilo alipokutana na Menejimenti na Watumishi wa Mfuko huo akiwa katika ziara yake ya kikazi na kujitambulisha kufuatia uteuzi uliofanywa na Rais Dr. John Magufuli hivi karibuni ambapo Naibu Waziri huyo alihamishiwa katika Wizara hiyo.

Naibu Waziri huyo amesema pamoja na mafanikio makubwa ambayo Mfuko huo umeyapata katika kuhudumia takribani Kaya Milioni Moja na Laki Moja za Wananchi wanaoishi katika umaskini, haupaswi kubweteka kwani suala la kupambana na Umaskini ni agenda muhimu katika Mipango ya Serikali ambayo pia imeainishwa kupitia ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi.

Aidha Dr.Mwanjelwa ameagiza Watumishi wa TASAF kuwa Wabunifu na kufanya kazi kwa karibu zaidi na Wananchi hususani walioko katika Mpango ili Matokeo ya utekelezaji wa Shughuli za miradi yawe endelevu na yanayopimika ili hatimaye kero ya umaskini miongoni mwa Wananchi iweze kupunguzwa kama siyo kumalizika kabisa.

Akizungumzia utekelezaji wa shughuli za Miradi ya Ajira ya Muda, Naibu Waziri huyo wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ameagiza TASAF kuhakikisha kuwa miradi inayotekelezwa kupitia utaratibu huo ni ile inayowanufaisha wananchi na malipo yafanywe kwa kuzingatia kanuni na taratibu za Serikali.

Wakati huo huo Dr. Mwanjelwa ametoa rai kwa halmashauri za wilaya kusimamia kwa karibu miradi inayotekelezwa na TASAF kwenye maeneo yao na kuonya kuwa pale ambapo itadhihirika kuwa halmashauri inakiuka taratibu wa miradi hiyo hatua zitachukuliwa haraka iwezekanavyo dhidi ya wahusika .

Akitoa taarifa ya Utekelezaji wa Shughuli, Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF ,Bwana Ladislaus Mwamanga amesema Mfuko huo umeendelea kutekeleza Maagizo ya Serikali ya kusaidia jitihada za Serikali katika kupambana na Umaskini nchini kote .

Bwana Mwamanga amezitaja sekta za Elimu, Maji,Afya ,Barabara,hifadhi ya Mazingira, Mifugo, Kilimo na uzalishaji mali na ujenzi wa rasilimali watu kuwa miongoni mwa maeneo yaliyopewa kipaumbele tangu kuanzishwa kwa Mfuko huo takribani miaka 20 iliyopita miradi ambayo amesema imetekelezwa kwa mafanikio makubwa kwa kuwahusisha wananchi kwenye maeneo yao.

Mkurugenzi Mtendaji huyo wa TASAF amebainisha pia kuwa utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini licha ya changamoto kadhaa zilizotokana na ukubwa wa Mpango huo kumekuwa na mafanikio makubwa hususani katika kubadili fikra za Walengwa ambao kwa sasa wanaendelea kuboresha maisha yao kwa kutumia huduma za Mpango huo.Amesema maboresho muhimu yatafanywa kwa kuzingatia maelekezo ya Serikali ili katika sehemu ya pili ya Mpango inayotarajiwa kuanza hivi karibuni kuwa na ufanisi zaidi ikiwa ni pamoja na kuyafikia maeneo ambayo hayakupata fursa hiyo katika awamu ya kwanza.

pic1

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Dr. Mary Mwanjelwa(aliyeshika kipaza sauti) akizungumza na Watumishi wa TASAF (hawapo pichani) kushoto kwake ni Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Bwana Ladislaus Mwamanga.

pic2

Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF,Bw. Ladislaus Mwamanga (aliyesimama) akitoa taarifa kwa Naibu Waziri Dr. Mary Mwanjelwa wakati alipofanya ziara ya utambulisho kwa watumishi wa taasisi hiyo.

pic3

Picha ya Juu na Chini baadhi ya Watumishi wa TASAF wakimsikiliza Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Dr. Mary Mwanjelwa (hayupo pichani) ambaye alifanya ziara katika taasisi hiyo.

 pic4

pic5

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Dr. Mary Mwanjelwa (aliyeketi katikati ) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Watumishi wa TASAF alipofanya ziara ya kujitambulisha .