• Print

User Rating: 1 / 5

Star ActiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
 

Wajumbe wa kamati ya Baraza la wawakilishi ya kusimamia ofisi za viongozi wakuu ya baraza la wawakilishi – Zanzibar wameanza ziara ya siku mbili ya kutembelea baadhi ya miradi inayotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii –TASAF- kwa lengo la kujifunza utendaji kazi wa mfuko huo ambao pia hutekeleza miradi yake huko Unguja na Pemba.

Wakiwa katika ofisi za Makao makuu ya TASAF wajumbe hao wamepewa taarifa ya miradi iliyotekelezwa na taasisi hiyo tangu kuanzishwa kwake mwaka 2000.Katika taarifa hiyo jumla ya miradi ya maendeleo 12,347 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 430 imetekelezwa kote nchini kwa kuwashirikisha wananchi .

Akizungumza katika kikao hicho Mwenyekiti wa kamati hiyo,Mhe. Omar Seif Abed amesema kazi zilizofanywa na TASAF zimeibua hamasa kwa wananchi kujiletea maendeleo na kupongeza utaratibu wa Mfuko huo kuwashirikisha wananchi katika uibuaji na utekelezaji wa miradi kwenye maeneo yao.

Aidha Mwenyekiti huyo ametoa changamoto kwa TASAF kuona namna inavyoweza kufuatilia miradi iliyoitekeleza hata baada ya kuwakabidhi wananchi au halmashauri ya wilaya ili iwe endelevu.

Wajumbe hao watapata fursa ya kutembelea miradi ya TASAF katika halmashauri ya wilaya ya Kibaha, mkoani Pwani ambako watakutana na baadhi ya walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.

Zifuatazo ni baadhi ya picha za Wajumbe wa Kamati hiyo walipokuwa katika kikao Makao Makuu ya TASAF

pic1

Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Mr.Ladislaus Mwamanga akiwakaribisha Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar TASAF Makao Makuu

pic2

Wajumbe wa Kamati ya Baraza la Wawakilishi Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wakipitia taarifa ya Utekelezaji wa Miradi ya TASAF 

pic3

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Kisiwani Zanzibar Mhe. Mihayo Juma Nhunga aliyesimama akitoa nasaha katika ziara ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi waliotembelea Makao Makuu ya TASAF jijini Dar es Salaam kuona utekelezaji wa shughuli za Mfuko huo.

pic4

Mkurugenzi wa Kujenga Uwezo wa TASAF, Mr. Amadeus Kamagenge aliyesismama akitoa  taarifa ya Utekelezaji wa Miradi ya Mfuko huo kwa Wajumbe wa Kamati ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar.