Mkurugenzi  Mkazi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa -USAID, Andy Karas amefanya ziara katika mkoa wa Kagera na kukagua shughuli zinazofanywa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF na kuridhishwa na maendeleo yaliyofikiwa katika utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini mkoani humo.

Akiwa katika kijiji cha Mishenyi kata ya Butelankuzi wilaya ya Bukoba Vijijini ,Mkurugenzi Mkazi huyo wa USAID alitembelea Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ambako alijionea namna Walengwa hao walivyoboresha makazi yao kwa kujenga nyumba bora kwa kutumia ruzuku itolewayo na TASAF .

Aidha Karas alipata ushuhuda wa Walengwa namna wanavyotumia ruzuku hiyo katika kuboresha huduma za elimu na afya kwa kaya zao huku pia wakitilia mkazo suala la uanzishwaji wa miradi midogo midogo ya uzalishaji mali kwa lengo la kujiongezea kipato chao.“huu ni mwelekeo sahihi na unaopaswa kuungwa mkono na wapenda maendeleo kama USAID kwani unatekelezwa kwa misingi endelevu” alisisitiza Mkurugenzi Mkazi huyo wa USAID.

Katika hatua nyingine Mkurugenzi Mkazi huyo wa USAID alikagua miradi na bidhaa mbalimbali inayotekelezwa na Walengwa wa Mpango wa kunusuru Kaya Maskini katika kijiji cha Mishenyi kama njia mojawapo ya kujiongezea kipato na kukuza uchumi wao. Miongoni mwa bidhaa hizo ni mbuzi, kuku,vikapu, mayai,vikapu na Mikungu ya ndizi.

Nao Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika kijiji hicho cha Mishenyi waliipongeza serikali kwa kubuni Mpango huo kupitia TASAF ambao wamesema umesaidia kurejesha utu wao kwani hapo awali waliishi katika hali ya ufukara na sasa wanaona nuru ikiwarejea kwa kuanza kumiliki mali na kumudu kuendesha maisha yao kaya zao.

Akizungumza katika hafla hiyo Mkurugenzi wa Miradi wa TASAF,Amadeus Kamagenge,aliwahakikishia walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini nchini kote kuwa Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii imeweka mkakati madhubuti wa kuwashirikisha walengwa katika kupunguza umaskini huku mkazo ukiwa ni kwa wao kufanya kazi za uzalishaji mali.

Zifuatazo ni picha za tukio hilo.

 pic1

Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Misaada la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa ,USAID, Andy Karas akikagua moja ya mabanda ya kufugia mbuzi lililoanzishwa na mmoja wa Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini, katika kijiji cha Mishenyi wilaya ya Bukoba mkoani Kagera kama njia mojawapo ya kujiongezea kipato.

pic2

Mkurugenzi  Mkazi wa USAID  Andy Karas  na Mkurugenzi wa Miradi wa TASAF Amadeus Kamagenge wakiangalia bidhaa zilizotengenezwa na Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika kijiji cha Mishenye kata ya Butelankuzi halmashauri ya wilaya ya Bukoba mkoani Kagera.

pic3

Mkurugenzi  Mkazi wa USAID  Andy Karas (aliyeshika daftari) akiangalia bidhaa zilizotengenezwa na walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaoratibiwa na TASAF  katika kijiji cha Mishenyi  kata ya Butelankuzi wilaya ya Bukoba mkoani Kagera kama njia mojawapo ya kujiongezea kipato na kupambana na umaskini.

pic4

Mkurugenzi Mkazi wa USAID  Andy Karas (wanne kulia )katika picha ya pamoja na Mkurugenzi wa miradi wa TASAF Amadeus Kamagenge (wa pili kulia )nje ya nyumba iliyojengwa na mmoja wa Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kwa kutumia fedha za Mpango huo  katika kijiji cha Mishenye kata ya Butelankuzi wilaya ya Bukoba mkoani Kagera.

pic5

Hapa ni mwendo wa zawadi tu, Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaoratibiwa na TASAF katika kijiji cha Mishenye kata ya Butelankuzi wilaya ya Bukoba mkoani Kagera wakimpatia zawadi mgeni wao Mkurugenzi Mkazi wa USAID baada ya kuzungumza nao na kuwatia moyo wa kufanya kazi ili waweze kuondokana na umaskini.