TASAF YAKUTANA NA WADAU WA MAENDELEO KUJADILI MPANGO WA KUNUSURU KAYA MASKINI.

Menejimenti ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii - TASAF imekutana na Wadau wa Maendeleo kujadili masuala mbalimbali ya utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaohudumia takribani kaya Milioni Moja na Laki Moja nchini kote.

Akitoa taarifa katika kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bwana Ladislaus Mwamanga amesema hatua kubwa imepigwa katika utekelezaji wa Mpango huo huku akiishukuru Serikali na  Wadau wa Maendeleo kwa kuendelea kutoa msaada muhimu katika kufikia mafanikio hayo.

Aidha Bwana Mwamanga amesema msaada wa Serikali na Wadau wa Maendeleo unaoendelea kutolewa umeusaidia kwa kiwango kikubwa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii – TASAF kuandaa kwa ufanisi Awamu ya Pili ya Mpango huo inayotarajiwa kuanza hapo mwakani.

Amesema maandalizi hayo yanazingatia kwa kiwango kikubwa maelekezo ya Serikali yanayosisitiza umuhimu wa walengwa kufanya kazi za uzalishaji mali ili hatimaye waweze kuondokana na umaskini na kuboresha maisha yao.

Bwana Mwamanga amesema TASAF imekuwa ikitiwa moyo na namna Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wanavyoendelea kutumia fursa hiyo muhimu ya kujumuishwa kwenye Mpango kwa kuzingatia masharti ya Mpango huo.

Vikao vya pamoja kati ya menejimenti ya TASAF na Wadau wa Maendeleo hufanyika kwa lengo la kuona namna shughuli za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini zinavyotekelezwa ili kukidhi matakwa na maagizo ya serikali ya kuhakikisha kuwa kero ya umaskini miongoni mwa walengwa inatokomezwa.

Zifuatazo ni picha za kikao hicho

pic1

Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw. Ladislaus Mwamanga (mbele) akiongoza kikao cha wadau wa maendeleo na menejimenti ya TASAF.

pic2

Wajumbe wa kikao cha menejimenti ya TASAF na Wadau wa maendeleo wakifuatilia mjadala kwenye kikao chao cha kila mwezi kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa TASAF.

pic3