Habari
Kamati ya Bunge yaipongeza TASAF kwa utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo

Kamati ya Kudumu ya Bunge, Utawala Katiba na Sheria imeupongeza Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF kwa utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo inayoboresha upatikanaji wa huduma za kijamii na ustawi wa maisha kwa jamii zenye uhitaji.
Akizungumza wakati wa ziara ya kamati hiyo iliyofanyika Mkoani Tanga katika wilaya ya Muheza, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Dkt Joseph Mhagama alisema utekelezaji wa miradi ya TASAF unafanyika kwa kuzingatia viwango na mahitaji ya jamii husika.
“Miradi ya TASAF inafanyika kwa ubora na ufanisi mkubwa, tunashudia jinsi wananchi na jamii zetu zinavyonufaika na miradi hii, tunaipongeza TASAF kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za kuleta maendeleo,” alisema wakati kamati hiyo ilipotembelea ujenzi wa vyumba sita vya madarasa, jengo la utawala na matundu 6 ya vyoo katika Shule ya Sekondari Magila iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Muheza.
"TASAF imeonesha ufanisi mkubwa katika kutekeleza miradi ya maendeleo, hasa katika maeneo ya Muheza na Bagamoyo. Miradi hii inatoa mchango mkubwa katika kuboresha maisha ya wananchi, ikiwa ni pamoja na kuongeza upatikanaji wa huduma bora za kijamii na kupunguza umasikini. Hii ni ishara ya mafanikio ya TASAF katika utekelezaji wa mipango yake ya maendeleo".
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deus Sangu alisema utekelezaji wa miradi ya TASAF unalenga kurahisisha upatikanaji wa huduma bora za kijamii kwenye maeneo yenye uhitaji.
Mhe. Sangu, aliahidi kuwa TASAF itaendelea kutekeleza miradi ya maendeleo ili kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma bora za kijamii na kupunguza umaskini.
Huu ni uthibitisho wa juhudi za Serikali katika kuboresha maisha ya wananchi, na ni matumaini kuwa TASAF itaendelea na juhudi zake hizo kwa manufaa ya watu wengi.
“Miradi hii inayotekelezwa inaendelea kuboresha maisha ya wananchi kwa njia ya kipekee, na tunahakikisha kwamba TASAF itaendelea kufanya kazi nzuri ya kuleta maendeleo na huduma bora kwa wananchi,” alisema.
Kati ya Mwezi Machi 2021 hadi Februari mwaka 2025, jumla ya shilingi Bilioni 31.4 zimetolewa na TASAF kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Mkoani Tanga, fedha hizo zimetumika katika utekelezaji wa kiradi ya Miundombinu pamoja na ruzuku kwa wanufaika wa Mpango.