Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Ikulu

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii

Habari

TASAF yazindua malipo kwa walengwa wanaoishi kando ya barabara za Mwendo Kasi


Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF umezindua zoezi la malipo kwa walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya za Walengwa wanaoishi kwenya nyumba za kupanga zilizopo kando ya barababara za mabasi ya mwendokasi kwa lengo la kuwafanya  wanufaike na fursa mbalimbali za kiuchumi  zilizopo katika maeneo yao.

Zoezi hilo linalotekelezwa katika Wilaya za Ilala, Ubungo na Kinondoni, lilizinduliwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila ambaye aliipongeza TASAF kwa utekelezaji thabiti wa Mpango wa Kunusuru Kaya za Walengwa.

Mhe. Chalamila pia aliwasihi wanufaika wa Mpango waliopokea ruzuku hiyo kuitumia ipasavyo na kuhakikisha wanatimiza malengo ya kujiinua kiuchumi kwa kuchangamkia fursa mbalimbali za maendeleo zilizoletwa na ujenzi wa miradi ya barabara za mwendo kasi.

“Serikali inafanya jitihada nyingi za kuboresha maisha ya wananchi kwa kuboresha upatikanaji wa huduma za kijamii, miongoni mwa juhudi zilizofanyika ni pamoja na ujenzi wa Miradi ya Barabara za Mwendo Kasi. Miradi hii imesababisha kupanda kwa gharama za maisha hivyo kusababisha ugumu wa maisha kwa wananchi wenye  hali duni,” alisema.

“Ninaipongeza TASAF kwa kutekeleza zoezi hili ambalo lina umuhimu mkubwa kwa ustawi wa maisha ya wananchi hasa walengwa wa Mpango wanaoishi kando kando ya barabara za mwendokasi ili waweze kuendelea kumudu gharama ya maisha ma kunufaika na fursa mbalimbali za biashara na maendeleo zilizopo,” aliongeza.

Awali, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Bw. Shedrack Mziray, Meneja wa Miradi ya Ajira za Muda na  Uendelezaji wa Miundombinu Bw. Paul Kijazi, alisema Mpango huu unasaidia kaya za walengwa zilizo hatarini kushindwa kumudu kuishi karibu na njia ya Mwendokasi kutokana na kupanda kwa gharama za maisha, ikiwemo kodi ya nyumba. Pia unalenga kuwawezesha wakazi wa mijini wenye kipato cha chini kunufaika na fursa za kiuchumi zinazotokana na mfumo wa mabasi yaendayo haraka.

Ili kufanikisha hili, wanufaika hupokea ruzuku ya kodi ya nyumba, mafunzo ya ujasiriamali, ushauri wa kibiashara, na mwongozo wa mabadiliko ya kitabia. Hatua hizi zinawawezesha kuendelea kuishi katika makazi yao licha ya kupanda kwa gharama za maisha na kunufaika na fursa zinazopatikana.

“Mpango huu, unaotekelezwa na TASAF, ulianza kwa utambuzi na usajili wa Kaya Maskini katika mitaa ya wilaya tatu, sambamba na utambuzi wa mafunzo ya msingi ya ujasiriamali,” alisema.

Jumla ya wanufaika 1,535 wa Mpango wa Kunusuru Kaya za Walengwa walitambuliwa ili kushiriki katika Mpango wa majaribo wa kutoa ruzuku ya ziada jumla ya kaya 1,023 zilitengwa kwa ajili ya kupata hafua za mpango, na kaya 511 ni za mlinganisho.