Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Ikulu

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii

Habari

Benki ya Dunia yafurahishwa Ruzuku ya Uzalishaji Rungwe


Wadau wa Maendeleo ikiwemo Benki ya Dunia wamefurahishwa na jinsi Ruzuku ya Uzalishaji inavyowanufaisha Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe na kuwapongeza kwa jitihada wanazozifanya katika kupunguza umaskini.

Walengwa wa Rungwe ambao wamepata ruzuku ya uzalishaji wameonesha uwezo mkubwa na ubunifu wa hali ya juu katika kuitumia ruzuku hiyo kuanzisha miradi yenye manufaa na kujiongezea vyanzo vya mapato katika kaya zao.

Hayo yamedhihirika wakati Timu ya Tathmini iliyoongozwa na mwakilishi wa Benki ya Dunia ilipofika wilayani Rungwe kujionea namna ruzuku hiyo inavyowanufaisha Walengwa wa Mpango huo.

Akijinasibu mbele ya Timu ya Tathmini iliyofika nyumbani kwake kuona namna alivyoitumia ruzuku ya uzalishaji aliyoipata, Bi. Freda Michael Adamson (38) wa Kijiji cha Isebelo Kata ya Swaya wilayani Rungwe amesema kuwa ruzuku za TASAF ambazo amekuwa akipokea zimempaisha kimaisha na kumfikisha katika viwango ambavyo haikuwa rahisi kwa hali ya kawaida kuvifikia.

“Mimi hapa kijijini nilikuwa maskini wa kutupwa ndo maana hata TASAF walipofika kuandikisha kaya maskini wanakijiji wakisoma niandikishwe ili baadaye Serikali ikatutupe kwenye Ziwa Ngosi maana tumekuwa kero hapa kijijini”, alieleza kwa uchungu sana Bi. Freda, akiongeza, “Leo nimekuwa miongoni mwa watu maarufu na matajiri wa kijiji hiki cha Isebelo maana hali yangu ya maisha imeboreshwa na TASAF na kunifanya niwe mtu kati ya watu”.

Bi. Freda amesema kuwa kwa sasa fedha ndogo ndogo hazimpigi chenga kwa kuwa ana vyanzo vingi vya kipato maana mpaka sasa TASAF imemwezesha kuwa na ng’ombe watatu wa maziwa, nguruwe wanne, kuku 12, amepanda miche 100 ya parachichi ambapo kwa mwaka huu ameanza kuvuna, ameuza na kupata Tsh. 1,000,000/=; amelima viazi eka moja na nusu, anategemea kupata gunia 80 ambapo atauza kila gunia kwa wastani wa 45,000 na kupata takribani 3,500,000/=.

Bi. Freda Michael Adamson akiwa mbele ya banda la ng’ombe wa maziwa katika Kijiji cha Isebelo Kata ya Swaya, Wilaya ya Rungwe

“Mbali na hayo, nimejenga nyumba ya kisasa, nimeweka sola, king’amuzi na televisheni kwa ajili ya kujua dunia inakwendaje, nina migomba ya ndizi kwa ajili ya chakula na sasa nawaza kumiliki gari kwa ajili ya kusafirishia mazao”, alitamba Bi. Freda.

Kwa upande mwingine Bi. Freda amewashukuru maafisa ugani kwa kuwa wamekuwa bega kwa bega kuwahudumia wakati wote bila kuchoka na kwa wakati.

“Kwenye kijiji chetu cha Isabelo mlezi wetu wa TASAF na Afisa Ugani Bw. Mawazo Mwasanguti kila ukimpigia simu anakuja kwa wakati na hadai chochote, anahudumia mifugo yetu bure kabisa. Mungu ambariki sana kwa majitoleo yake kwetu Walengwa wa TASAF”, alisema Bi. Freda.

Kwa upande Mwingine, Bi. Sauda Mwamboneka (37) naye ni Mlengwa wa TASAF aliyepata ruzuku ya uzalishaji katika Kijiji cha Katumba Kata ya Ibighi, Wilaya ya Rungwe. Yeye anaishukuru TASAF kwa sababu kupitia ruzuku hiyo pamoja na ruzuku nyingine ameweza kununua ng’ombe wawili (2) wa kisasa huku akiendeleza mradi wake wa kufuga nguruwe, kilimo cha mbogamboga na matunda anavyoviuza katika genge lake lililopo sokoni Katumba.

“Mbali ya hayo niliyoyasema, nimejenga nyumba ya kisasa, nimeingiza maji, umeme, ninasomesha watoto wangu wawili na ninamiliki ekari mbili za migomba na ninamlea mama yangu mzazi ambaye ni mgonjwa”, alisema Bi. Sauda.

Bi. Sauda Mwamboneka akiwa katika mabanda yake ya nguruwe na ng’ombe aliyoyajenga kwa ruzuku za TASAF katika Kijiji cha Katumba Kata ya Ibighi, Wilaya ya Rungwe

Naye Atupele Kingi Mwasomola ambaye pia ni Mlengwa wa TASAF na mmoja wa waliopokea ruzuku ya uzalishaji amesema pamoja na ruzuku za TASAF alizokuwa akipokea tangu atambuliwe na kuandikishwa kwenye Mpango mwaka 2015, ruzuku ya uzalishaji imempigisha hatua kubwa sana maana ameweza kuanzisha mradi wa kufuga nguruwe ambapo anazalisha vitoto na kuuza kila kimoja kwa Tsh.50,000/=.

“Mradi wa nguruwe niliouanzisha baada ya kupata ruzuku ya uzalishaji umeniongezea ujanja wa kiuchumi maana nilikuwa na kijumba cha hovyo hovyo lakini sasa nimejenga nyumba nzuri, kubwa na ya kisasa yenye choo ndani, nimeingiza maji, umeme na nina king’amuzi kwa ajili ya kuangalia taarifa mbalimbali. Pia nauza kuni zinazonisaidia kupata fedha ndogo ndogo kwa mahitaji ya kila siku, Mungu anipe nini?” alisema Bi. Atupele.

Bi. Atupele Kingi Mwasomola akiwa mbele ya nyumba yake ya kisasa aliyoijenga kwa ruzuku za TASAF katika Kijiji cha Katumba Kata ya Ibighi, Wilaya ya Rungwe

Akizungumza na Walengwa zaidi ya 20 waliopokea ruzuku ya uzalishaji mali, mwakilishi wa Benki ya Dunia Bw. Stanley Magesa amekiri kufurahishwa na namna Walengwa wanavyojitahidi kutumia kwa ubunifu ruzuku wanazopata.

“Kwa jitihada hii ambayo tumeiona hapa Rungwe, na kwa mifano ambayo tumeiona kwenye vijiji vya Katumba na Isebelo, naomba kuwapongeza sana kwa jitihada mnazozifanya kujikwamua kutoka kwenye umaskini, nina uhakika mtafika mbali sana. Tumewasikiliza maelezo yenu nyote, tumeona kazi inayofanywa na Sauda Mwamboneka, Atupele Kingi Mwasomola na Freda Michael Adamson, hakika mmefanya kazi kubwa na wengine wanapaswa kuja kujifunza kutoka kwenu maana kazi yenu ni njema sana”, alizungumza Bw. Stanley Magesa.

Timu ya Tathmini inafanya ziara katika maeneo mbalimbali ya utekelezaji ambayo Walengwa wake wako kwenye vikundi na wamepokea ruzuku za uzalishaji ili kujifunza namna wanavyopambana na kuondokana na umaskini uliokithiri katika kaya zao. Baadhi ya maeneo ya utekelezaji yaliyokwisha kufikiwa ni pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino (Dodoma), Halmashauri ya Wilaya ya Singida (Singida) na Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi (Mwanza).